Kwa mujibu wa ripoti ya Kitengo cha tarjuma cha Shirika la Habari la Hawza, Jumuiya ya “Al-Wefaq Al-Watani Al-Islami” nchini Bahrain imesisitiza kwamba; utawala umechukua hatua ambayo imeielezea kuwa ni “hatari na ya kulazimisha,” kwa kuivunja taasisi ya “Waqfu wa Jaafari” na kuiunganisha ndani ya baraza linalohusishwa na mamlaka ya kisiasa, Jumuiya hiyo imeichukulia hatua hiyo kuwa ni uvunjaji wa hukumu za kisheria za dini, ukiukwaji wa katiba, pamoja na uvamizi dhidi ya mila na desturi zinazohusiana na uhuru wa kidini nchini humo.
Al-Wefaq ilitangaza kwamba; mwenendo huu ni uvamizi ambao haujawahi kushuhudiwa nchini Bahrain au katika nchi nyingine yoyote katika kipindi cha mamia ya miaka iliyopita. Kwa mujibu wa jumuiya hiyo, utawala umetumia vibaya mazingira ya eneo, migogoro na vita, kwa ajili ya kunyakua na kuingilia mamlaka, viongozi, taasisi pamoja na mali za madhehebu ya Jaafari, hatua hii inafanywa kupitia mbinu za mabavu zinazojengwa juu ya vitisho na kueneza hofu, aidha sheria zinabadilishwa kwa lengo la kulazimisha hali halisi ambayo iko kinyume na dini, maandiko ya Qur’ani na sheria za Kiislamu, pamoja na utambulisho wa kimadhehebu na uhuru wa umma na binafsi.
Jumuiya hiyo iliongeza kwamba; hatua hizi ni ukiukaji wa wazi na usiovumilika wa misingi ya sheria za dini, na kwamba zimeambatana na kampeni za kiusalama pamoja na kuundwa kwa mazingira ya hofu na vitisho kwa lengo la kuwazuia wananchi kutoa malalamiko au kupinga hatua hizo.
Jumuiya ya Al-Wefaq ilieleza kuwa; utawala uliandaa mazingira ya hatua hizi zisizo za kisheria kupitia kulazimisha hali inayofanana na kutangazwa kwa hali ya hatari pamoja na kuimarisha mazingira ya kiusalama.
Kwa mujibu wa taarifa ya Jumuiya ya Al-Wefaq, mazingira haya yalianza kwa kuuawa kishahidi Sayyid Muhammad Al-Mousawi chini ya mateso na kukabidhiwa mwili wake ukiwa na alama za mateso zilizoonekana wazi. Kisha yakafuatiwa na kuvuliwa uraia familia zote na kulazimishwa kuhama kwao, pamoja na kukamatwa kwa makumi ya wanazuoni kutoka mikoa na maeneo mbalimbali ya Bahrain na kusambazwa kwa picha zao kwa namna ambayo jumuiya hiyo imeitaja kuwa ni aina ya kulipiza kisasi. Pia ilielezwa kuhusu kuondolewa kwa maimamu wa swala katika makumi ya misikiti, pamoja na kufungwa kwa shule, hawza na mimbari za kidini.
Jumuiya ya Al-Wefaq inaamini kwamba; hatua hizi zinaonesha kuwa, yaliyotokea ni maandalizi ya kushambulia hali halisi ya kidini na kijamii, kufunga taasisi, kunyakua mali na kubadilisha mfumo wa usimamizi wake kuwa “usimamizi wa kiusalama wa ukandamizaji” unaoendeshwa kwa misingi ya kimadhehebu na usiozingatia misingi ya sheria za dini, kijamii, kisheria na kibinadamu.
Jumuiya ya Al-Wefaq ilibainisha kwamba amri namba (31) ya mwaka 2026 ni uamuzi wa kisiasa wenye lengo la kuvunja taasisi hiyo, ambao umelazimishwa kwa nguvu, uamuzi huo si tu kwamba umelenga taasisi yenye asili ya kihistoria nchini Bahrain, bali pia unakusudia kuleta mabadiliko ya kulazimishwa ambayo yatazalisha mgogoro mkubwa wenye mizizi ya mamia ya miaka.
Jumuiya hiyo iliongeza kuwa; historia itarekodi hatua hii kuwa kosa kubwa zaidi la utawala wa Bahrain, na ikasisitiza kwamba hali hii haiwezi kupatana na maumbile ya mwanadamu, dini, uhuru na sheria.
Jumuiya ya Al-Wefaq ilisisitiza kwamba; amri hii ya kulazimishwa ni usaliti na unyakuzi wa maelfu ya waqfu ambazo zimewekwa kwa majina na mifumo maalumu ya waqfu, na ambazo hazikubali kufanyiwa mabadiliko wala kuingiliwa kisiasa.
Jumuiya hiyo ilisisitiza kwamba; waqfu haibadilishwi kwa amri au uamuzi wa serikali, na kwamba hatua zote zilizochukuliwa ni batili na hazina uhalali wa kisheria wala wa kidini.
Al-Wefaq ilitoa wito kwa utawala kufuta amri hiyo na kuacha ubabe, ukaidi na kung’ang’ania kuendeleza mradi ambao hauwezi kuendelea isipokuwa kwa kutumia nguvu, vitisho na kwenda kinyume na hukumu za sheria za dini.
Jumuiya hiyo inaamini kwamba; kulenga waqfu wa Mashia na Sunni kupitia kulazimisha hali ambayo kwa mtazamo wa kidini haikubaliki, kunathibitisha umuhimu wa kufafanua upya mfumo wa kisiasa wa nchi hiyo, kwa sababu mfumo uliopo umepoteza vipengele vya ushirikiano, uhalali na kuishi pamoja.
Al-Wefaq ilitoa wito wa kuandaliwa “mkataba mpya wa kijamii” unaojengwa juu ya misingi ya kisheria na ya wananchi, ambao utatoa dhamana zinazohitajika kwa watu binafsi na makundi mbalimbali na kuimarisha hali ya utulivu na uhakika kuhusu maisha yao ya sasa, mustakabali wao, utambulisho wao pamoja na uhuru wao.
Maoni yako